Wasanii Wakongwe Waungana Kuadhimisha Miaka 30 ya Bongo Fleva
Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva Lazinduliwa Rasmi Dar es Salaam
Wasanii wa Bongo Fleva nchini wameandaa tamasha maalumu kwa ajili ya kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa muziki huo uliobeba historia kubwa ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki.
Tamasha hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City Julai 10, 2026 na linatarajiwa kuwakutanisha wasanii wakongwe waliotikisa miaka ya nyuma pamoja na kizazi kipya cha muziki wa Bongo Fleva.
Lengo kuu la tamasha hilo ni kuwakumbusha mashabiki kuwa muziki wanaoufurahia sasa umejengwa juu ya msingi uliowekwa na wasanii wa mwanzo wa Bongo Fleva.
Leo Mei 21, 2026 katika ukumbi wa Hayat Hotel jijini Dar es Salaam, wasanii mbalimbali walijitokeza kuunga mkono uzinduzi wa tamasha hilo huku baadhi yao wakizungumza kuhusu historia na mustakabali wa muziki huo.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Muziki Tanzania ambaye pia ni msanii, Fid Q, amesema moja ya changamoto zinazoufanya muziki wa Tanzania kushindwa kufanya vizuri kwenye tuzo kubwa za kimataifa kama Grammy ni kupoteza utambulisho wa asili wa Bongo Fleva.
“Bongo Fleva ya zamani ilikuwa na utambulisho wa kipekee uliobeba lugha, tamaduni na simulizi za maisha ya Mtanzania. Muziki wa mwanzo ulielezea maisha halisi ya mtaani, ndoto, changamoto na matumaini ya jamii,” amesema Fid Q.
Hata hivyo, Fid Q amesema baadhi ya wasanii wa sasa wamejikita zaidi katika kuiga mitindo ya kimataifa kama Amapiano na Afrobeats badala ya kujenga sauti yao binafsi ya Kitanzania.
Kwa upande wake, Mratibu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva, Madee Ali, amewataka wasanii wa zamani kuacha kuitwa wakongwe kwa sababu wao ndio msingi wa muziki huo nchini.
Msanii Chid Benz amesema umoja huo ni njia nzuri ya kuwaweka pamoja wasanii wa aina mbalimbali huku kizazi kipya kikijifunza kutoka kwa wakubwa wao walioweka historia kwenye muziki wa Tanzania.
Mastaa waliojitokeza kwenye uzinduzi huo ni pamoja na Afande Sele, Mr Blue, Chid Benz, Dully Sykes, Fid Q, Madee Ali, Feruzi, Loud Eyz na wengine wengi.
Endelea kufuatilia IddyNation kwa habari zote za Bongo Fleva, mastaa wa Tanzania na burudani za Afrika Mashariki.

No comments
Note: only a member of this blog may post a comment.