-->

Breaking News

Filamu 65 Kuchuana Kuwania Tuzo Katika Tamasha la ZIFF 2026 Zanzibar

Filamu 65 Kuchuana Kuwania Tuzo Katika Tamasha la ZIFF 2026 Zanzibar

Jumla ya filamu 65 zimechaguliwa kuwania tuzo katika Tamasha la 29 la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF 2026) litakalofanyika kuanzia Juni 24 hadi 28, 2026 visiwani Zanzibar.

Filamu hizo zimechaguliwa kutoka zaidi ya filamu 400 zilizowasilishwa kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa ajili ya kushiriki katika tamasha hilo kubwa la filamu Afrika Mashariki.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya tamasha hilo, Mkurugenzi wa ZIFF, Hatibu Madudu, amesema mwaka huu wamepokea filamu nyingi kutoka Afrika Mashariki huku Uganda ikiongoza kwa kuwasilisha filamu 50, Tanzania 45 na Kenya 23.

Nchi nyingine zilizowasilisha filamu nyingi ni pamoja na Afrika Kusini, Nigeria, Iran, Marekani, India, Brazil, China, Korea Kusini, Ufaransa, Uingereza na mataifa mengine duniani.

Madudu amesema filamu zilizochaguliwa zinajumuisha filamu ndefu 14, filamu za makala 13, tamthilia za televisheni 10, filamu fupi 22 pamoja na filamu sita za animesheni.

Makundi ya ushindani mwaka huu ni pamoja na Filamu Bora Ndefu, Filamu Bora Makala, Filamu Bora Afrika Mashariki, Muigizaji Bora wa Kiume na wa Kike pamoja na tuzo maalum za Zanzibar na Chaguo la Watazamaji.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale, amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Akili Unde (AI) na Sanaa ya Usimuliaji wa Hadithi”.

Amesema AI inaleta mapinduzi makubwa katika utengenezaji wa maudhui ya filamu, lakini Afrika bado inakabiliwa na changamoto za miundombinu, ukosefu wa data za ndani na upungufu wa wataalamu wa teknolojia hiyo.

ZIFF 2026 pia itatoa mafunzo maalum kuhusu matumizi ya AI katika utengenezaji wa filamu, elimu ya fedha kwa watengenezaji wa filamu na mbinu za usambazaji wa maudhui ya kidijitali.

Baadhi ya wataalamu watakaoshiriki kutoa warsha ni pamoja na Lisa Russell, mshindi wa tuzo ya Regional Emmy pamoja na Balozi wa Women in AI nchini Kenya.

Tamasha hilo linatarajiwa kuvutia zaidi ya watazamaji 200,000 kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki huku likiendeleza utamaduni wa sinema na usimuliaji wa hadithi kupitia filamu.

Endelea kufuatilia IddyNation kwa habari zote za filamu, burudani na matukio makubwa ya sanaa Afrika.

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.

🔔 Enable Notifications

Get latest songs and entertainment updates instantly.