Travis Scott Afika Mahakamani Kupinga Kesi ya Mauaji, Ahoji Matumizi ya Mashairi ya Rap
Travis Scott Afika Mahakamani Kupinga Matumizi ya Mashairi ya Rap Katika Kesi ya Mauaji
Rapa maarufu wa Marekani Travis Scott pamoja na wasanii wengine wa hip hop wamewasilisha hoja muhimu katika Mahakama Kuu ya Marekani wakipinga matumizi ya mashairi ya rap kama ushahidi katika kesi ya mauaji.
Wasanii walioungana naye ni pamoja na Killer Mike, T.I., Young Thug, Fat Joe na N.O.R.E., wakidai kuwa matumizi ya mashairi hayo yanaweza kuchochea ubaguzi wa rangi na kuathiri haki ya mshtakiwa kupata kesi ya haki.
Kesi hiyo inamhusu James Garfield Broadnax, ambaye alihukumiwa kifo mwaka 2009 baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji yaliyotokea Texas mwaka 2008.
Katika kesi hiyo, waendesha mashtaka waliwasilisha mashairi ya rap yaliyoandikwa na Broadnax kama sehemu ya ushahidi, jambo ambalo sasa linapingwa vikali na wanamuziki hao.
Kwa mujibu wa hoja ya kisheria iliyowasilishwa, matumizi ya mashairi ya rap kama ushahidi ni kinyume cha Katiba ya Marekani, hasa kipengele kinacholinda uhuru wa kujieleza.
“Kuadhibu mtu kwa sababu ya maandishi yake ya rap ni sawa na kuadhibu aina ya sanaa na kujieleza,” ilieleza sehemu ya hoja hiyo.
Kesi hii imeibua mjadala mkubwa duniani kuhusu nafasi ya muziki wa rap katika mfumo wa sheria na haki za wasanii, huku wengi wakitaka mabadiliko ya sheria ili kulinda ubunifu na uhuru wa kujieleza.



No comments
Note: only a member of this blog may post a comment.