-->

Breaking News

Bien anavyopewa heshima kwenye Bongofleva

 Bien anavyopewa heshima kwenye Bongofleva

PETER AKARO

Mwimbaji wa zamani wa kundi la Sauti Sol kutokea Kenya, Bien (38), anaendelea kupata heshima kubwa ndani ya Bongofleva kwa jinsi ambavyo amekuwa akipewa nafasi na wasanii wa muziki huo pendwa nchini.

Bien, mkali wa kibao cha Too Easy (2023), tayari ameshirikiana na wasanii wote wakubwa Bongo ambao wanafanya vizuri kwa wakati huu, jambo linaloonyesha nguvu ya ushawishi wake.

Tayari amefanya kazi na majina mengi makubwa, baadhi yao ni Alikiba (Finale), Diamond Platnumz (Katam), Darassa (Nobody), Harmonize (I Made It), Joh Makini (Formula) na Marioo (Nairobi).

Wengine ni Jux (Lucky Now), Rayvanny (Rakata) na Nandy (Kiza Kinene), mwanzilishi wa The African Princess Label, ambaye walishirikiana akiwa na Sauti Sol.



Bien alikuwa miongoni mwa waimbaji wanne waliounda kundi la Sauti lililoanzishwa mwaka 2005 jijini Nairobi likipiga muziki wa Afropop. Waimbaji wengine ni Willis Chimano, Savara Mudigi na Otieno, mpiga gitaa aliyejiunga nao baadaye.

Ndani ya kundi hilo, Bien alisimama kama mwimbaji kiongozi na mtunzi mkuu wa nyimbo, kwa kifupi alikuwa mhimili muhimu katika ukuaji wa Sauti Sol hadi kuwa moja ya makundi yenye mafanikio barani Afrika.

Sauti Sol walipata umaarufu kutokana na mtindo wao wa kuchanganya muziki wa jadi Kenya na Afropop pamoja na R&B. Nyimbo zao maarufu ni kama Still The One (2013), Sura Yako (2013), Kuliko Jana (2016), Melanin (2017), Suzanna (2020) n.k.

Baada ya mafanikio makubwa wakifanya ziara nyingi Afrika, Ulaya na Amerika, mnamo Mei 2023, Sauti Sol walitangaza kuchukua likizo ya muda mrefu ili kutoa nafasi kwa kila mmoja kufanya kazi zake binafsi, yaani solo.

Na hapo ndipo Bien alipoanza kuvuma zaidi peke yake akipata mafanikio makubwa ya kibiashara kupitia albamu yake ya kwanza, Alusa Why Are You Topless? (2023) yenye nyimbo 16 huku akishirikiana na wasanii wakubwa kama Ayra Starr kutokea Nigeria.

Wakati huu ndipo jina la Bien lilianza kuchukua nafasi kubwa katika muziki Bongo akipewa kolabo nyingi, kitu kinachoendelea hadi sasa huku wanachama wenzake wa Sauti Sol wakiwa hawapati fursa hiyo.

Ni hivi karibuni ameachia kolabo yake na Staa wa Bongofleva kutokea Kings Music, Alikiba, Finale (2026) ambayo imeanza kupata mapokezi mazuri. Hii ni mara ya pili kwa wawili hao kushirikiana baada ya hapo awali kukutana katika ngoma ya Sauti Sol, Unconditionally Bae (2016).

Ushirikiano huu mpya ni uthibitisho mwingine kuwa Bien anakubalika ndani ya Bongofleva, na yeye pia anaikubali Bongofleva na ndio sababu hata kolabo zake nyingi na wasanii wa hapa zimekuwa na matokeo mazuri.

Mara ya mwisho Bien alikuwa ameshirikiana na Marioo katika wimbo wake 'Nairobi' kutoka katika albamu yake ya pili, The God Son (2024) chini ya Bad Nation Label.

Wimbo huo uliotayarishwa na Kaniba ndio uliofanya vizuri zaidi katika albamu hiyo, hadi mwishoni mwa 2025 video yake ilikuwa imetazamwa YouTube mara milioni 44 ikiwa ni video ya pili ya Bongofleva iliyofanya vizuri zaidi kwa mwaka huo nyuma ya 'Pawa' yake Mbosso.
Kolabo nyingine iliyobamba kati ya Bien na msanii wa Bongo, ni ile alivyofanya na rapa kutokea Classic Music Group (CMG), Darassa, Nobody (2023) uliyotayarishwa na Abbah.

Ngoma hiyo imesikilizwa (streams) mara milioni 18 katika mtandao wa Boomplay Music, na ndio wimbo wa kwanza wa rapa huyo kufikia namba hizo tangu alipotoka rasmi kimuziki na wimbo wake, Sikati Tamaa (2012) akimshirikisha Ben Pol.

Akiendelea kusimamia peke yake kama msanii wa kujitegemea, mwimbaji, mtunzi wa nyimbo na mpiga gitaa, Bien anazidi kujenga himaya yake Afrika Mashariki hasa kwao Kenya, na Tanzania.

Julai 2024, Bien aliachia toleo lingine (deluxe) la albamu yake, Alusa Why Are You Topless? (2023), ambapo aliwashirikisha wasanii kama Fally Ipupa (DR Congo) na Adekunle Gold (Nigeria).

Bien akiwa ni mwanzilishi mwenza wa lebo ya muziki ya Sol Generation Records, muziki wake umepata mafanikio makubwa ya kibiashara - mwaka 2024, Spotify ilimtaja kuwa msanii wa Kenya aliyesikilizwa zaidi.

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.

🔔 Enable Notifications

Get latest songs and entertainment updates instantly.