-->

Breaking News

Baada ya Diamond kutoa Happy, TID atia neno


 RHOBI CHACHA


Lejendari wa Bongofleva, Khalid Mohamed maarufu kisanii kwa jina la TID ameibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuzungumzia mwenendo wa utoaji wa nyimbo mpya kufuatia kuachiwa kwa wimbo wa 'Happy' wa Diamond Platnumz.

Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho kumeshuhudiwa msururu wa nyimbo mpya kutoka kwa wasanii wakubwa hali inayotafsiriwa kuwa ushindani wa karibu unaolenga kuvuta hisia za mashabiki ndani ya muda mfupi.

Kupitia maelezo yake, TID ameeleza kuwa mara nyingi wasanii hujikuta wakivutiwa na nguvu ya kutrendi inayotengenezwa na msanii mkubwa, jambo linalowafanya wengine pia kuachia kazi kwa wakati ili wasiachwe nyuma kimtazamo wa mashabiki.

"Kila mtu anafuraha lakini mimi nataka niseme kitu kimoja, kama Diamond asingetoa huu wimbo wa 'Happy', naamini kabisa wengine wasingetoa nyimbo zao muda huu huu, wanachofanya ni kutumia trend ili wao pia waonekane," ameandika TID kwenye akaunti yake ya instagram.

Ingawa hakumtaja msanii yeyote moja kwa moja, kauli hiyo imekuja sambamba na kuachiwa kwa nyimbo mpya za wasanii wengine wakubwa ndani ya muda mfupi, ambapo baadhi zimetoka zikipishana kwa siku mbili hadi tatu tu.

Kwa upande wa mashabiki, maoni yamegawanyika; wapo wanaokubaliana na mtazamo huo wakidai kuwa trend ina nafasi kubwa kwenye mafanikio ya kazi za muziki, huku wengine wakisisitiza kuwa kila msanii ana uhuru wa kutoa kazi yake muda wowote kulingana na mipango yake.

Hata hivyo, kinachoendelea kwa sasa kinaonesha wazi kuwa ushindani ndani ya Bongofleva umefikia hatua nyingine, huku kila msanii akipambana kuhakikisha anabaki relevant na kuvuta hisia za wapenzi wa muziki.

Kwa hali ilivyo, kauli ya TID imeendelea kuwa gumzo, huku wengi wakifuatilia kwa karibu kuona namna kazi hizo mpya zitakavyofanya sokoni.

Baada ya Diamond Platnumz kutoa wimbo wa Happy, siku chache Harmonize ametoa wimbo wa 'Wewe' huku Ali Kiba akiachia wimbo wa 'Finale' alioshirikishwa na Bien msanii kutoka Kenya.

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.

🔔 Enable Notifications

Get latest songs and entertainment updates instantly.