Peter Akaro
Mwanamitindo maarufu duniani, Kendall Jenner (29) ameweka wazi mpango wa kuachana na kazi yake hiyo pamoja na maisha ya umaarufu, akieleza kuwa sasa anataka kuishi maisha ya kawaida na kujikita katika shauku yake kubwa ya kubuni na kusanifu majengo.
Jenner aliyeanza kujulikana akiwa na umri wa miaka 11 kupitia kipindi cha familia yake, Keeping Up With The Kardashians, amesema licha ya familia yake kusaini mkataba mnono na kampuni ya Hulu kuendeleza reality show hiyo, yeye binafsi hajawahi kuvutiwa sana na maisha ya kuwa mbele ya kamera kila wakati.
Katika mahojiano na Jarida la Vogue wiki hii, Jenner amesema anapenda maisha ya kawaida yanayompa uhuru wa kuamka asubuhi na kuvaa nguo ya kuogelea au suruali ya mazoezi bila kupaka vipodozi usoni na kuishi maisha yake kutwa nzima akiwa hivyo.
"Naapa kwa Mungu, nitaacha kila kitu na kujikita katika kazi ya kubuni na kusanifu majengo. Sisemi hili kwa mzaha," alisema Jenner katika mahojiano hayo akiwa pamoja na Gigi Hadid, mwanamitindo na mtangazaji wa televisheni huko Marekani.
Mrembo huyo ambaye ni mtu wa 13 duniani kuwa na wafuasi (followers) wengi katika mtandao wa kijamii wa Instagram, ameongeza kuwa anaipenda zaidi hali ya maisha ya kawaida kuliko mwonekano wa kifahari kutoka tasnia ya mitindo.
"Naipenda nyumba yangu kule Los Angeles, lakini pia napenda maisha rahisi. Napenda kuamka kila asubuhi na kufanya mambo yangu kutwa nzima bila kuzuizi chochote. Nafikiria sana kuhusu maisha yajayo, lakini hujaribu kutopanga kupita kiasi kwa sababu unajua mimi ni mtu wa kupanga sana mambo," alisema Jenner.
Alisema anapenda kujiona wa kawaida zaidi siku ambazo hayupo katika shughuli zake za mitindo jukwaani, hivyo hujitahidi kufanya mambo ya tofauti kidogo ili kufurahia maisha katika hali ya kawaida kama watu wengine.
"Napenda kwenda kwenye mashindano ya mbio za farasi nikiwa nimevaa kama watu wengine nikivaa kofia yangu, miwani ya jua na sare yangu, na ninaweza kushiriki mbizo hizo kwa kutumia jina tofauti kabisa na watu wasijue," alieleza.
Katika mahojiano ya awali na Emma Chamberlain kupitia podcast ya Anything Goes hapo Agosti 2024, Jenner alizungumzia maisha yake ya shule na changamoto za umaarufu wa familia yake.
"Tulienda shule kadiri tulivyoweza. Hivyo, ingawa tulikuwa na kipindi cha televisheni nyumbani, tulikuwa tunaenda shule za kawaida mchana kutwa na tulikuwa na marafiki tuliokuwa nao kabla kipindi hakijaanza.
"Haikuwa rahisi kila wakati, lakini mpangilio huo ulinifanya nijisikie kuwa kawaida. Kwa ujumla, ninashukuru sana kwa sababu nafikiri mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi," alisema Jenner.
Alisema yeye na mdogo wake Kylie waliendelea kuwa imara bila kuyumbishwa na umaarufu kwa sababu ya upendo wa familia na mwongozo waliopewa na dada zao wakubwa ambao wana uzoefu katika tasnia hiyo.
"Nadhani mimi na Kylie, jambo moja tulilokuwa nalo ni uthabiti mkubwa mambo yanayokuja mbele yetu, upendo mwingi na mfumo mzuri wa kusaidiana pamoja na marafiki wazuri tulionao," alieleza Jenner.
Ikumbukwe Jenner kwao walizaliwa wawili tu ila baada ya familia yao 'kuungana' na ile ya Kardashian, wakapata ndugu wengine kama Kourtney, Khloe, Rob na Kim, mwanamitindo bilionea na mke wa zamani wa rapa Kanye West (Ye).