A Zeno.FM Station Baltasar Engonga Ebang Ahukumiwa Miaka 18 Jela…

Baltasar Engonga Ebang Ahukumiwa Miaka 18 Jela…


Baltasar Engonga Ebang, aliyewahi kushikilia wadhifa wa juu kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Fedha la Equatorial Guinea, amehukumiwa kifungo cha miaka 18 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma. Hukumu hiyo ilitolewa na mahakama ya kitaifa kufuatia mchakato wa muda mrefu wa kisheria ulioibua taarifa nyingi za kushangaza kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, ulaji rushwa, na mienendo isiyo ya kimaadili kwa kiongozi huyo wa zamani.

Kwa mujibu wa nyaraka za mashitaka na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Engonga alituhumiwa kutumia zaidi ya Sh milioni 209.3 kutoka kwa hazina ya serikali kwa ajili ya matumizi yake binafsi ya kifahari. Fedha hizo zilitumika kwa shughuli zisizo za kiofisi, zikiwemo kuhudumia wake na wake wa watu, kununua zawadi za thamani kubwa, kulipia vyumba vya hoteli vya kifahari, na anasa nyingine zisizo na maelezo ya kiofisi. Kiasi kingine cha zaidi ya Sh milioni 20 kilipotea bila maelezo ya kutosha, kikihusishwa na safari za siri na matumizi ya starehe.

Mashitaka yaliyowasilishwa dhidi ya Engonga yalikuwa na uzito mkubwa na yalihusisha vipengele vitatu vikuu:

  1. Ubadhirifu wa mali ya umma – miaka 8 jela,
  2. Kujitajirisha kinyume cha sheria – miaka 4 na miezi 5,
  3. Matumizi mabaya ya mamlaka – miaka 6 na siku moja.

Jumla ya kifungo chake kilifikia miaka 18, huku upande wa mashitaka ukisisitiza kwamba hukumu hiyo ni mfano kwa viongozi wengine wanaotumia nyadhifa zao kwa faida binafsi.

Mbali na mashtaka ya kifedha, Engonga pia alihusishwa na kashfa kubwa ya video chafu, iliyozua taharuki si tu nchini Equatorial Guinea bali hata katika jumuiya ya kimataifa. Mnamo Novemba 2024, mitandao ya kijamii ilisambaza video zaidi ya 400 zikimuonyesha Engonga akijihusisha na vitendo vya ngono na zaidi ya wanawake 40. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba video hizo zilinaswa katika maeneo ya hadhi ya juu kama ofisi ya serikali, hoteli za kifahari, kwenye magari ya serikali, na hata maeneo ya wazi kama kando ya mito.

Wanawake wengi waliotajwa kuhusika walikuwa wake za viongozi wa serikali, ndugu wa watu maarufu, na baadhi walikuwa wafanyakazi wa karibu wa Engonga. Ripoti zinaeleza kuwa aliwalaghai kwa kutumia ushawishi wa madaraka yake na mara nyingine kuwatishia kwa kutumia taarifa alizokuwa nazo kupitia nafasi yake ya kikazi. Pia inasemekana Engonga ana watoto sita kutoka kwa wanawake tofauti, wengi wao wakiwa walihusiana naye kupitia mazingira ya kazi au kisiasa.

Kufuatia kashfa hiyo ya video chafu, serikali ilichukua hatua za haraka kujaribu kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi zake. Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo alimteua Zenón Obiang Obiang Avomo kuchukua nafasi ya Engonga kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Fedha. Hatua hiyo ilipokelewa kwa mchanganyiko wa hisia huku baadhi ya wananchi wakihimiza uchunguzi zaidi na wengine wakitaka viongozi wote waliokuwa karibu na Engonga pia wachunguzwe.

Engonga, ambaye mara kadhaa amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa watu waliokuwa na ushawishi mkubwa ndani ya serikali, sasa anakabiliwa na maisha ya gerezani yaliyotangazwa kuwa yatahusisha utengwaji maalum kutokana na hatari za usalama wake binafsi. Pia amepigwa marufuku kushika wadhifa wowote wa umma au usimamizi wa fedha kwa kipindi kisichopungua miaka 25 baada ya kutumikia kifungo chake.

Hukumu ya Engonga ni moja ya matukio makubwa zaidi ya kisiasa na kisheria kuwahi kutokea nchini Equatorial Guinea katika miaka ya hivi karibuni. Inaonyesha mwelekeo mpya wa taifa hilo katika kupambana na rushwa, pamoja na kurejesha nidhamu na maadili kwa viongozi wa umma. Hata hivyo, waangalizi wa masuala ya kisiasa wanashauri kuwa jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha kwamba adhabu kama hii haiwi ya mtu mmoja tu bali inakuwa mfumo wa kweli wa kuwajibisha watumishi wote wa umma.

Post a Comment

0 Comments