Zuchu: Sina Kinyongo na Gigy Money
Zuchu Amsamehe Gigy Money Baada ya Kuombwa Radhi Hadharani
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Zuchu amesema tayari amemsamehe msanii mwenzake Gigy Money kufuatia tofauti zilizowahi kujitokeza kati yao siku za nyuma.
Zuchu amesema hana kinyongo chochote dhidi ya Gigy Money na anaamini ugomvi ni sehemu ya maisha ya kawaida, hivyo hakuna sababu ya kuendeleza chuki.
Akizungumza na waandishi wa habari Posta jijini Dar es Salaam, Zuchu alisema tayari alikuwa amemsamehe Gigy hata kabla hajamuomba radhi hadharani kupitia mitandao ya kijamii.
“Kwanza nilishamsamehe tangu zamani, na isitoshe ameenda hadi mtandaoni kuniomba radhi. Hata mimi ni mtu mwepesi wa kumuomba mtu msamaha pale ninapokosea,” alisema Zuchu.
Msanii huyo pia alisema anamuheshimu Gigy Money kwa hatua aliyochukua ya kuomba radhi hadharani, akieleza kuwa si kila mtu ana uwezo wa kufanya jambo hilo.
“Tunazungumza kama kawaida kwa sababu sisi ni vijana na bado tunahitajiana. Sina kinyongo kabisa, kwani hata juzi alinipigia simu na tukazungumza kwa muda mrefu,” aliongeza.
Mahusiano ya wawili hao yaliwahi kuzua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kurushiana kauli katika nyakati tofauti, lakini kauli ya Zuchu inaonekana kuweka wazi kuwa tofauti hizo sasa zimefikia mwisho.
Wiki moja iliyopita, Gigy Money aliomba msamaha kupitia ukurasa wake wa Instagram akisema anatamani kuweka mambo sawa kati yao.
“Natumaini uko salama na unaendelea vizuri. Nimechukua muda kuandika ujumbe huu kwa moyo wa kweli na unyenyekevu,” aliandika Gigy Money.
Pia alisema kuwa kama kuna sehemu yoyote alimkwaza au kumuumiza Zuchu, anaomba asamehewe kwa dhati kabisa.
“Siombi ili nirudishe yaliyopita kwa lazima, bali nataka moyo wangu uwe safi mbele yako na mbele ya Mungu,” aliongeza.
Endelea kufuatilia IddyNation kwa habari zote za Bongo Fleva, mastaa wa Tanzania na burudani za Afrika Mashariki.
No comments
Note: only a member of this blog may post a comment.