-->

Breaking News

Mahakama ya rufaa yaanza kuhoji hukumu ya Diddy

 Mahakama ya rufaa yaanza kuhoji hukumu ya Diddy

Mahakama ya Rufaa Nchini Marekani imeanza kuhoji kifungo cha takriban miaka minne alichopewa mkali wa Hip Hop na Mfanyabiashara maarufu kutoka Marekani Sean ‘Diddy’ Combs kama ni kikubwa kupita kiasi.

Katika usikilizwaji wa hoja uliofanyika New York, Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa hawakutoa uamuzi wa haraka lakini walionesha kuwa kesi hiyo ni ngumu na ya kipekee ambapo Jaji William J. Nardini alieleza kuwa kesi hiyo inaleta maswali mapya ambayo hayajawahi kujadiliwa kwa kina katika Mahakama za shirikisho.

Wakili wa Diddy, Alexandra Shapiro, alidai kuwa Mteja wake alipewa hukumu ndefu zaidi kuwahi kutolewa kwa mtu mwenye makosa kama yake katika historia ya nchi hiyo, huku akisisitiza kuwa Jaji alikosea kwa kuzingatia mambo yanayohusiana na makosa ambayo Diddy aliachiliwa huru nayo, jambo ambalo halipaswi kuathiri hukumu.

Katika hoja zilizowasilishwa katika mahakama hiyo, mawakili wa Diddy walisisitiza kuwa Jaji wa kesi alizingatia mambo ambayo hayakupaswa kuathiri hukumu ikiwemo madai ya udanganyifu na shinikizo ambalo kwa mujibu wao tayari lilishakataliwa awali.

Kwa upande wa mashtaka ulitetea hukumu hiyo ukisema ilikuwa ndani ya mipaka ya sheria na ilizingatia mienendo ya mshtakiwa kwa ujumla kauli ambayo ilifanya baadhi ya majaji waanze kuitilia shaka mantiki hiyo wakihoji iwapo ni sahihi kuongeza uzito wa adhabu kwa kutumia ushahidi ambao haukusababisha hatia katika mashtaka makubwa yaliyokuwa yakimkabili.

Kwa ujumla, mjadala huo unaonyesha uwezekano wa mabadiliko ya hukumu iwapo Mahakama ya Rufaa itaona kulikuwa na makosa katika namna adhabu ilivyopimwa ambapo uamuzi wa mwisho unaweza kuthibitisha kifungo hicho, kukipunguza au kuamuru kusikilizwa upya kwa suala la adhabu kulingana na tafsiri sahihi ya sheria.

Ikumbukwe Diddy alikamatwa Septemba 16, 2024 jijini New York akikabiliwa na mashtaka mazito ikiwemo racketeering na usafirishaji wa watu kwa ajili ya ngono, ambapo baada ya kesi kusikilizwa mwaka 2025 baadhi ya makosa yalitupiliwa mbali lakini alipatikana na hatia kwa makosa mawii ya kusafirisha watu kwa ajili ya ukahaba chini ya sheria ya Mann Act.

Oktoba 3, 2025 alihukumiwa kifungo cha miaka minne na miezi miwili jela, aidha rufaa yake ya kupinga adhabu hiyo ilikubaliwa mapema mwezi huu, ambapo mahakama ya rufaa ilianza kusikiliza hoja zake bila kutoa uamuzi wa mwisho hadi sasa.

Sean 'Diddy' Combs kwa sasa anatumikia kifungo chake katika gereza la FCI Fort Dix lililopo New Jersey

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.

🔔 Enable Notifications

Get latest songs and entertainment updates instantly.