-->

Breaking News

Janet Jackson hayupo kwenye filamu ya maisha ya MJ

 Janet Jackson hayupo kwenye filamu ya maisha ya MJ

Wakati zikiwa zimebaki siku 13 kabla ya kuachiwa filamu ya wasifu wa mfalme wa Pop marehemu Michael Jackson, taarifa mpya zimeibuka zikidai kuwa kwenye filamu hiyo baadhi ya wanafamilia hawakuhusishwa kabisa.

Filamu hiyo iliyopewa jina la Michael, ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu, inalenga kusimulia safari ya kipekee ya msanii huyo kuanzia utotoni hadi kuwa mmoja wa wasanii wakubwa kuwahi kutokea duniani.


Kwa mujibu wa chanzo kilichoiona filamu hiyo, dada yake Michael, Janet Jackson, ambaye pia ni nyota muziki Marekani, hajaonyeshwa kabisa katika filamu hiyo. Hatua ambayo imezua maswali kwa mashabiki wengi, hasa kutokana na nafasi aliyokuwa nayo Janet wakati MJ akipambania ndoto zake.

Ikumbukwe Janet alikuwa mlezi na mshauri mkubwa wa MJ huku akipanga matamasha na kusafiri naye sehemu mbalimbali ambazo alikuwa akienda kwa ajili ya kazi za kimuziki.

Aidha mbali na Janet, dada yao mkubwa Rebbie Jackson, naye hakupewa nafasi ya maana katika filamu hiyo, huku La Toya Jackson akionekana katika scene mbili tu.

Licha ya hayo, kundi maarufu la familia hiyo, The Jackson 5, lilionekana ndani ya filamu, hasa katika hatua za mwanzo za maisha ya Michael alipokuwa akianza safari yake ya muziki akiwa mtoto. Licha ya kundi hilo kuonekana lakini Michael ndio alikuwa akipewa kipaumbele Zaidi.



Kwa upande wa uandaaji wa filamu, imeripotiwa kuwa Janet Jackson hakuwa miongoni wa waandaji wakuu na badala yake walitumika baadhi ya ndugu zake akiwemo Jermaine Jackson, Tito Jackson, Jackie Jackson, Marlon Jackson, La Toya pamoja na mtoto wa MJ, Prince Jackson kukamilisha filamu hiyo.

Filamu ya Michael inatarajiwa kuonesha si tu mafanikio ya msanii huyo, bali pia changamoto, migogoro na maisha yake binafsi yaliyojaa mafumbo mengi. Hii ndiyo sababu imekuwa ikitajwa kuwa moja ya filamu kubwa zaidi za wasifu kuwahi kutengenezwa Hollywood.



Michael Jackson alizaliwa mwaka 1958 na kufariki dunia mwaka 2009. Amewahi kutamba na ngoma kama Smooth Criminal, Thriller, na Will You Be There ambazo zimeendelea kukusanya watazamaji kila iitwayo leo katika chati za muziki.

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.

🔔 Enable Notifications

Get latest songs and entertainment updates instantly.