-->

Breaking News

Uadui wa Koffi Olomide na binti yake Didi Stone ulianzia huku!

 Uadui wa Koffi Olomide na binti yake Didi Stone ulianzia huku!

Nevumba Abubakar

Kila lilipotajwa jina la Didi Stone Olomide halikukosekana kuwepo Koffi Olomide, mwanamuziki nguli wa rhumba nchini DR Congo aliyetikisa Afrika na duniani kwa miongo kadhaa.

Ukaribu wao uliwafanya wengi kuwaona kama mfano wa uhusiano imara na maelewano mazuri kati ya mzazi na mtoto ndani ya familia ya watu maarufu.

Lakini kama unavyojua watu wanaopendana mara nyingi wanakosana, wanagombana na muda mwingine kuchukiana. Ndivyo ilivyotokea kwa Koffi na mwanaye kipenzi Didi upendo huo uligeuka maumivu na mtafaruku wa kifamilia usiotarajiwa.



Mwananchi inakuletea simulizi ya binti aliyewahi kuwa nguzo kwa baba yake lakini sasa anatajwa kuwa upande tofauti kabisa na kuibua mjadala mkubwa kuhusu uaminifu, haki na nafasi ya mtoto katikati ya migogoro ya wazazi.

ALIKUWA NGUZO KWA KOFFI
Kwa miaka kadhaa mtoto huyo alionekana kuwa karibu sana na baba yake labda kwa sababu ni moja ya watu maarufu na yupo mitandaoni kuliko wenzie.

Katika matukio mengi ya muziki, mitandaoni, mitindo na maisha Didi alikuwa akimuunga mkono Koffi Olomide, akimtaja kama mfano wake mkubwa kwenye tasnia na maisha.

Wengi waliona kama uhusiano wa kipekee kwa mtoto wa mwanamuziki maarufu kujivunia mafanikio ya baba yake na kusimama naye bila kuyumba.

"Baba yangu amekuwa kila kitu kwangu. Nimejifunza mengi kutoka kwake na nitabaki kumheshimu," aliwahi kunukuliwa akisema katika moja ya mahojiano.

TALAKA ILIVYOHARIBU
Kinachotajwa uhusiano huo kuvunjika na kuchangia hadi Didi kuwa mbali na baba yake ni baada ya kuvunjika kwa ndoa ya Koffi na Aliane ambaye ni mama yake mzazi.

Taarifa za kuvunjika kwa ndoa hiyo zilivyosambaa hali ya uhusiano wa kifamilia ilianza kuyumba hasa kwa Didi ambaye inaelezwa baada ya kujua hilo linaenda kutokea akavunja mawasiliano.

Katika kipindi hiko mwanamitindo huyo alianza kuonyesha dalili za kubadilika kwenye mitazamo yake na akaacha kumsifia baba yake kwenye mikutano mbalimbai hasa baada ya madai mbalimbali kuibuka kuhusu chanzo cha mgogoro huo.

Inaelezwa Koffi alikuwa na uhusiano wa muda mrefu na aliyekuwa msanii wake, Cindy Le Coeur ambaye alijiunga na Quartier Latin mwaka 2007.

Koffi alikuwa na uhusiano wa kimya kimya na msanii huyo ambaye sasa amefunga naye ndoa ya kiserikali Februari 28, 2026.

Baada ya mama yake Didi ambaye ni mwanamitindo wa zamani wa Ufaransa kugundua hilo mwaka 2021 aliomba talaka licha ya kudumu kwenye ndoa yao kwa takribani miaka 27.

Oktoba 2022 wakapeana talaka katika mahakama ya Bobigny, Ufaransa, miaka miwili baadae Koffi alithibitisha hadharani kuwa ameachana na Aliane na akatangaza kutoka kimapenzi na Cindy.

ABADILI UPANDE
Mara baada ya Didi kujua baba yake alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine akaamua kusimama upande wa mama yake tangu kesi ya talaka imeanza hadi walipotalikiana.

Hali hiyo ilionekana kama pigo kwa Koffi Olomide, hasa ikizingatiwa ukaribu waliokuwa nao awali.

"Nimechagua kusimama na mama yangu kwa sababu naamini anahitaji nguvu na msaada zaidi katika kipindi hiki na nafahamu amekosewa sana hivyo nipo naye bega kwa bega," anaeleza.

Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa mitandaoni, baadhi wakimuunga mkono kwa uamuzi wake na wengine wakimkosoa kwa kuonekana kumgeuka baba yake kwa kosa moja.

DIDI STONE MWENYEWE
Didi Stone alizaliwa Julai 17, 1999 huko Marseille, Ufaransa na ni mtoto wa kwanza wa wanandoa, Aliane mwanamitindo wa zamani nchini humo na Koffi.

Katika familia hiyo walizaliwa wawili na mdogo wake Del Pirlo ambao wote walikulia Ufaransa na DR Congo ambako waliishi na ndugu zao wengine wa kambo Aristotle na Minou, hawa ni watoto wa Marianne, pia walikuwepo Rocky, Diego na Karine ambao ni watoto Stephanie.

Baada ya masomo ya sekondari, Didi alijiunga na chuo cha biashara, EBS Paris, European Business School ili kusomea biashara na mitindo na mwaka 2021 alihitimu ngazi ya shahada ya kwanza.



Inaelezwa tangu mdogo Didi alikuwa akipendelea mitindo fani aliyorithi kutoka kwa mama yake na alipofikisha miaka 15 mawakala mbalimbali wa mitindo kimataifa walitamani kufanya naye kazi.

Lebo yake ya kwanza kufanya kazi ni Next Management, Metropolitan Models Group kisha akasainiwa na Elite Modeling Management kampuni zote mbili zilifanikiwa kukuza chapa yake.

Alipofikisha umri wa miaka 16, Didi alitokea katika jarida la Vogue na tangu wakati huo ameonekana na kuhojiwa na majarida makubwa ya mitindo na maisha kama vile Vanity Fair, Paris Match, Grazia, The New York Times, Forbes n.k.

Aliandika rekodi ya kipekee kuwa mwanamitindo wa kwanza mdogo kutoka DR Congo kutokea kwenye majarida hayo makubwa ya mitindo.

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.

🔔 Enable Notifications

Get latest songs and entertainment updates instantly.