-->

Breaking News

Kina Travis Scott wapinga rap kutumika katika hukumu ya kifo!

 Kina Travis Scott wapinga rap kutumika katika hukumu ya kifo!

Peter Akaro

Rapa wa Marekani, Travis Scott pamoja na wenzake wameiomba Mahakama Kuu (Supreme Court of the United States) kupitia upya kesi ya mwanaume mmoja Mweusi aliyehukumiwa kifo, wakisema matumizi ya mashairi ya rap katika kesi hiyo ni kinyume cha Katiba.

Wasanii waliowasilisha hoja za kisheria kuunga mkono ombi hilo ni pamoja na Killer Mike, T.I., Young Thug, Fat Joe na N.O.R.E., wakidai kuwa mashairi hayo yalitumika kuchochea ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya muziki wa rap.



Kesi hiyo inamhusu James Garfield Broadnax ambaye mwaka 2009 alihukumiwa na jopo la majaji (karibia wote wazungu) kwa kosa la kuwaua wanaume wawili wakati wa tukio la wizi lililotokea mwaka 2008 huko Garland, Texas.

Baada ya kupatikana na hatia, waendesha mashtaka waliwasilisha mashairi ya rap yaliyoandikwa na Broadnax kama sehemu ya ushahidi wakati majaji walipokuwa wanaamua kama apewe hukumu ya kifo.

Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la The New York Times, majaji waliomba kuyapitia mashairi hayo yenye kurasa 40 mara mbili wakati wa majadiliano yao kabla ya kutoa hukumu.

Mawakili wa Broadnax mwezi uliopita waliiomba Mahakama Kuu ya Marekani kusimamisha utekelezaji wa hukumu yake ya kifo uliopangwa kufanyika mwezi ujao na pia kupitia upya kesi hiyo.

Katika hoja iliyowasilishwa na timu ya kisheria ya rapa Travis Scott, walieleza kuwa matumizi ya mashairi ya rap katika kesi hiyo yalikuwa kinyume cha katiba!.

"Waendesha mashtaka walidai kuwa Broadnax anaweza kuwa hatari siku zijazo kwa sababu tu aliandika gangster rap. Hoja kama hiyo kimsingi ni adhabu isiyo ya kikatiba inayolenga maudhui ya muziki wa rap kama aina ya kujieleza," ilisomeka sehemu ya hoja ya Scott.

Hoja yao pia ilisisitiza kuwa muziki wa rap, ambao kwa kiasi kikubwa hutengenezwa na kuhusishwa kihistoria na wasanii wa jamii za wachache, unalindwa na marekebisho ya kwanza ya katiba ya Marekani yanayolinda uhuru wa kujieleza.

Akizungumza na jarida la Rolling Stone, wakili wa Travis Scott, Ellyde R. Thompson, alisema kesi hiyo inahusu haki za msingi za kikatiba na kusisitiza kuwa hukumu ya kifo haipaswi kutegemea kazi ya kisanii inayolindwa na katiba.

Kwa upande mwingine, hati iliyowasilishwa na Killer Mike na wasanii wengine ilieleza kuwa mashairi ya rap mara nyingi ni hadithi za kubuni na si maelezo halisi ya maisha ya mwandishi. Hivyo, kuyatumia kama ushahidi wa tabia ya uhalifu ni tafsiri potofu ya sanaa hiyo.

"Kesi hii inaonyesha wazi ni kwa namna ubaguzi wa rangi unavyoathiri mchakato wa haki pale serikali inapoitumia rap katika mashtaka kuchochea chuki dhidi ya rap na dhidi ya watu Weusi," ilisema hati hiyo.

Wakili Chad Baruch alisema kesi hiyo inaweza kuwa fursa muhimu kwa Mahakama Kuu kuweka mipaka ya kisheria kuhusu matumizi ya kazi za kisanii kama ushahidi katika kesi za jinai.

Hata hivyo, mawakili wa jimbo la Texas wamepinga hoja hizo wakisema upande wa Broadnax ulichelewa kupinga matumizi ya mashairi hayo, na kudai kuwa yalitumika kwa sehemu ndogo tu katika hoja za upande wa mashtaka. Kwa sasa, Mahakama Kuu ya Marekani inatarajiwa kuamua kama itasikiliza kesi hiyo upya au la.

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.

🔔 Enable Notifications

Get latest songs and entertainment updates instantly.