Katikati ya Konde, Kajala, Marioo na Paula kuna pesa nyingi

Baba mkwe Konde Boy, ana pipo milioni 11 na laki 4. Mama Mkwe Kajala ana watu milioni 8 na laki 3. Marioo mkwewe ana milioni 6 na laki 3 ya watu. Paula bintiye ana milioni 2 na laki 5. Namba za watu wao Instagram haziongopi kabisa wana watu.
Hao wote wapo kwenye kurasa zao za Instagram tu. Achana na TikTok, YouTube na kwingineko. Tunafahamu asilimia kubwa ya watu wa Insta ndo waliopo TikTok na kwengineko. Tubaki na hao hao tu kwa sasa wanatosha sana kutupa hesabu ndefu tuitakayo.
Chukua hiyo milioni 11.4 + milioni 8.3 + milioni 6.3 + milioni 2.5 = milioni 35. Balaa! Hii ndo familia yenye ufuasi wa watu milioni 35 'keshi' Instagram pekee. Mitaani huku na kwingineko tunakuacha kwanza kwa leo, ili tudili na hao tu wa Insta, tusijipe kazi ngumu sana.
Unaweza kufuatiliwa na maelfu ya watu lakini siyo kwa wema. Hata wauaji, wala rushwa, vibaka na wauza dawa za kulevya nao hufuatiliwa. Lakini hawapendwi na zaidi hufuatiliwa ili wamalizwe katika jamii, wanachukiwa kama shetani na wafuasi wake.
Konde ni mwanamuziki mwenye jina kubwa na anapendwa. Kajala ni muigizaji mwenye jina kubwa na anapendwa. Marioo na yeye ni mwanamuziki jina kubwa sana na anapendwa. Paula ni mtoto wa mastaa wakubwa nchini P. Funk na Kajala. Na anapendwa.
Na mke wa staa kutoka Alooo! Anapendwa na Marioo. Ndiyo! Na anapendwa na mama yake. Yes! Na anapendwa na baba yake. Na ana mashabiki wanampenda na kumfuatilia. Utamueleza nini toto 'Pii' mwenye makuzi ya Bamaga pale Mwenge?
Umaarufu tu ni pesa na utajiri. Blue Ivy ni staa mkubwa duniani kwa sasa. Siyo mwanamuziki au muigizaji, ustaa wake unatokana na majina ya wazazi wake Jay Z na Beyonce. Toto linapiga madili mengi ya 'branding' kubwa kubwa za kutosha. Nomaaa!
Kajala kabla ya kuigiza alikuwa ni maarufu bila kipaji chochote. Pisi ya P Funk Majani, ilikuwa sababu kubwa ya umaarufu wake ingawa wengi hawakuijua sura na shepu. Muvi za Kanumba zikampa ustaa wa sura na umbile. Ghafla akawa muiguzaji staa.
Kajala anabaki kuwa mmoja wa mastaa wa kike, mwenye madili mengi ya ubalozi. Na kwenye hili pengine anafunika mastaa kibao wa 'muvi'. Ana mvuto binafsi na hata matukio yake ya maisha na mahaba huvutia wengi. Sijui ila ana nyota kali kuliko wengi.
Ndo maana 'kapo' yake na Konde hutikisa sana wakirudiana ama kuachana. Kwa sababu Kajala ni 'stori meka' mkubwa, kama enzi za Wema katika nyakati zake bora. Hawezi kuwa kama Wema, ila ni kama Wema kwa sasa hivi katika 'kumeki hedilaini'.
Tofauti kubwa ya Kajala na Wema iko hivi. Ustaa wa Kajala unaenda sawa na uvunaji wa pesa binafsi. Umaarufu wa Wema ulienda sawa na kutengeneza mastaa wengine. Na siyo kumuingizia pesa yeye kama yeye. Alitumika sana Wema katika wakati wake.
Kupitia Kajala, imefikia hatua na Konde anaongeza mashabiki wa nje ya jukwaa la muziki. Kupitia Marioo pia Paula ametengeneza mashabiki wengi kutoka kwenye jukwaa la muziki. Hapa hakuna wa kumvimbia mwenzake wote mastaa.
Ukiondoa Diamond Platnmuz, hii ndo familia iliyokusanya mastaa watupu. Pengine tofauti iliyopo ni kwamba, Mondi kaifanya familia yake iwe maarufu, wakati huku ni watu maarufu waliojenga familia moja. Tunaweza kusema hii ndo familia ya mastaa kweli.
Mondi familia ya supa staa, hii ni familia ya mastaa. Huku kila mtu na kwa wakati wake katengeneza 'bezi' ya 'fansi' wake. Wote wanne wana 'masozi' za kufanya kitu bila kumtegemea mwenzake. Kwa hili ni rahisi kutajirika sana kwa kutumia vipawa vya umaarufu.
Wanachokosa ni akili ya juu zaidi, itakayoifanya familia hii 'kumeki moo mane'. Una Konde na Kajala, Marioo na Paula. Unataka nini? Kosa hapa ni kushindwa kuigeuza familia hii kuwa mradi wa pesa nyingi kwa majina yao. Wanaishia kwenye 'komenti na laiki'
Kinachotukwamisha Wabongo ni matumizi sahihi ya bongo zetu tu. Wataishia kufungulia duka la nguo Paula. Na siyo kuuza nguo zenye jina la Paula. Kifupi Paula anapaswa kuuza 'brand' yake na siyo kuuza duka lake. Inahitajika akili ya juu zaidi.
Konde akiwa na meneja na Kajala anastahili meneja wake. Marioo akiwa na meneja, Paula anastahili meneja wake. Kituko ni kwamba Konde Boy atamgeuza Kajala awe meneja. Hii ni kwa sababu wengi tunaamini kazi ya meneja wa staa ni kutunza pesa. Kosa!
Meneja jukumu lake ni kuratibu na kusimamia mitikasi zote za msanii. Meneja kusimamia yaliyo nje ya kazi, ni makosa. Bongo hii mameneja husimamia hadi ndoa ya dada au mama wa msanii. Hii siyo sawa na limeegemea katika uswahili uliokithiri.
Akili kubwa ikisimama katikati ya Konde, Kajala, Marioo na Paula. Kuna pesa nyingi katika familia hii. Huhitaji nguvu nyingi wakati wanajitosheleza kwa mtaji watu. Ufuasi wa watu wengi walionao unakupa njia nyingi za kugeuza majina yao kuwa pesa ndefu.
No comments
Note: only a member of this blog may post a comment.