KAMATI ya Utendaji ya Yanga leo imekutana makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kujadili mradi wa ujenzi wa Uwanja.
Kikao hicho kimefanyika siku moja tu baada ya uongozi huo kukabidhiwa Hati ya kiwanja chao wanachotaka kuwekeza mradi huo kilichopo eneo la Jangwani, jirani na makao makuu ya klabu.
Makamu wa Rais wa klabu, Arafat Haji na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Gulamali hawakuhudhuria kikao hicho, lakini wakishiriki kwa njia ya mtandao.
Ikumbukwe jana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius John Ndejembi alikabidhi Hati ya kiwanja cha klabu hiyo wakati wa tamasha la kilele cha Wiki ya Mwananchi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Waziri Ndejembi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi ametimiza ahadi aliyotoa kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka Yanga Jumapili iliyopita alipozungumza na wanachama kupitia simu ya Rais wa klabu, Hersi Ally Said.



Akitoa shukrani kwa Waziri na Serikali kwa ujumla chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan — Hersi alisema kinachofuata ni ujenzi wa Uwanja na akamtambulisha Mfadhili wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed kuwa ndiye Mwekezaji wa ujenzi wa Uwanja huo.
Pamoja na hayo, Rais Samia pia alizungumza na wana Yanga jana kuwapongeza kwa tamasha zuri akiwa Kigoma kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotrajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Ikumbukwe Rais Dk. Samia ndiye aliyeagiza Yanga wapatiwe Hati hiyo mwaka juzi wakati alipowaalika Ikulu Jijini Dar es Salaam kuwapongeza kwa kuingia Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.