Chapa za Alikiba na Diamond Platnumz zimekuwepo kwa miaka mingi katika kilele cha mafanikio zikichangia katika ukuaji wa Bongofleva na kutengeneza fursa za kiuchumi kwa wawili hao na kuwafanya kuwa wanamuziki ghali.
Mastaa hao walioshirikiana katika wimbo wa Kigoma All Stars, Nyumbani (2013) na kuketi pamoja katika video ya wimbo wa Tundaman, Starehe Gharama (2011), wamekuwa wakishindanishwa na mashabiki, lakini wanatofautiana kama ifuatavyo:
1. Tayari Diamond ametoa albamu tatu, Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), A Boy From Tandale (2018), na EP moja, First of All (2022). Naye Alikiba albamu tatu, Cinderella (2007), Ali K 4Real (2009), Only One King (2021) na EP moja, Starter (2024).
Diamond ametoa albamu zake zote katika miaka inayogawanyika kwa mbili huku albamu zote za Alikiba zikitoka miaka isiyogawanyika kwa mbili. Na wote hawajawahi kutoa albamu au EP ndani ya mwaka mmoja, kwa kifupi anapeana nafasi.
2. Katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), Diamond ameshinda mara 22 akiwa ndiye msanii aliyebeba mara nyingi zaidi kwa muda wote. Alikiba anashika nafasi ya pili akiwa ameshinda tuzo 18 na mara ya mwisho alifanya hivyo kupitia wimbo wake, Mahaba (2023).
3. Vilevile Diamond amewahi kubeba saba za TMA kwa usiku mmoja, hiyo ilikuwa msimu wa 2014. Alikiba akajiribu kuivunja rekodi hiyo 2015 ila akaishia kubeba tano, na hata alipojaribu tena 2021 akaishia kubabeba tano.
4. Alikiba hajawahi kufungiwa wimbo wake na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kutokana na kukiuka maadili, wakati Diamond kafungiwa nyimbo mbili, Hallelujah (2017) na Waka (2017), pia video ya wimbo wake, Mtasubiri (2022) imefungiwa.
5. Diamond ni mwanamuziki wa pili aliyetazamwa zaidi YouTube barani Afrika nyuma ya Burna Boy kutokea Nigeria, ila Alikiba hayupo hata 10.4 bora ya waliotazamwa sana katika mtandao huo ulioanzishwa Februari 14, 2005 nchini Marekani.
6. Vilevile Diamond ndiye mwanamuziki pekee Afrika mwenye wafuasi (subscribers) wengi YouTube akiwa nao zaidi ya milioni 10, wakati Alikiba akiwa hayupo hata 10 bora Afrika na kwa Tanzania akiwa nje ya tano bora akiwa na wafuasi wake milioni 2.1. Hivyo staa huyo wa WCB Wasafi anakuwa mwanamuziki wa kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kupata tuzo tatu kutoka YouTube ambazo ni Silver Creator Award (kwa wafuasi 100,000) na Gold Creator Award (1,000,000).
7. Mwanamitindo na Miss XXL After School Bash 2010, Hamisa Mobetto hadi sasa ametokea katika video za nyimbo mbili za Diamond, Mawazo (2012) na Salome (2016), huku kwa Alikiba akitokea katika video moja, Dodo (2020).
8. Diamond ndiye msanii pekee Tanzania aliyesikilizwa (most streamed) mara nyingi zaidi katika jukwaa la Boomplay Music akiwa na streams zaidi ya milioni 550, huku Alikiba akishika nafasi ya saba kwa Tanzania akiwa na streams milioni 216.
9. Rekodi lebo ya Diamond, WCB Wasafi ina rekodi ya kusaini wasanii nane hadi sasa huku wa kike wakiwa wawili, Queen Darleen na Zuchu, wakati ile ya Alikiba, Kings Music ikisaini wasanii sita kwa ujumla na hakuna hata mmoja wa kike.
10. Diamond ameshirikiana na wasanii watano kutokea Marekani ambao ni Rick Ross (Waka - 2017), Ne-Yo (Marry You - 2017), Omarion (African Beauty - 2018), Alicia Keys (Wasted Energy - 2020) na Ciara (Low - 2025).
Ila Alikiba amefanya kolabo na msanii mmoja tu wa nchi hiyo, naye ni R Kelly katika katika mradi wa One8 uliokutanisha wasanii wakubwa Afrika akiwemo 2Face na Fally Ipupa, kisha kutoa wimbo wa pamoja, Hands Across The World ((2010).