CHANZO CHA PICHA,REUTERS
Bingwa wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia Beatrice Chebet ameshinda mbio za wanawake za mita 10,000 katika mashindano ya Riadha ya Dunia ya 2025 huko Tokyo, Japan, na kuipatia Kenya medali ya kwanza kwenye mashindano hayo.
Mkenya huyo alikimbia kwa kasi mzunguko wa mwisho na kuvuka mstari katika dakika 30 sekunde 37.61 na kukamilisha mkondo wa kwanza wa kile anachotumai kuwa wa mbio za mita 5,000-10,000 mjini Tokyo kuendana na mafanikio yake katika Michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka jana.
"Zilikuwa mbio ngumu, zenye kuhitaji ustadi wa juu lakini nilikimbia mbio za mita 800 za mwisho kwa bidii sana... akili yangu ilikuwa kana kwamba niko kwenye mbio za mita 1500," Chebet alisema.
"Ilinibidi kujitahidi zaidi na kujipa motisha lakini nilitaka medali hiyo ya dhahabu sana. Sijawahi kushinda dhahabu kwenye michuano ya dunia hivyo, nilikuwa na uhakika kwamba nilipaswa kuipata."
Nadia Battocletti wa Italia alimaliza wa pili na kujishindia medali ya fedha huku Gudaf Tsegay wa Ethiopia akichukua nafasi ya tatu.