Mkali wa Bongo Fleva, Barnaba Classic amepinga vikali madai ya kuwa mume bwege kwa mke wake, Raya The Boss.
Barnaba amesema ni kweli huwa msikivu kwa mkewe, lakini sio kuwa mume bwege wa kukubali kila kitu kibaya kinachofanyika na kushindwa kutoa kauli kama mume.
Alisema madai ya watu, wakati mwingine huwa anafanya kazi za nyumbani hilo ni kawaida kwani kuna muda mwingine mke wake huwa anakuwa amechoka hivyo hawezi kumlazimisha kufanya kazi.
“Jamani ni kweli wakati mwingine namsaidia mke wangu kazi za nyumbani, ila sio kuitwa mume bwege na wanaosema mume akimsaidia mke kazi za nyumbani ni bwege basi hao hawajui mapenzi na upendo kwenye mahusiano. Yaani huwezi ukamfanya mtoto wa watu kama punda, kama unajua kupika kwa nini usiingie jikoni kupika wakati mwingine ili kumpa pumziko mke wako? Watu tubadilike tuache ukoloni kwenye ndoa zetu au mahusiano yetu,” alisema Barnaba.
Barnaba aliendelea kumtetea mkewe ambaye inasemekana anampelekesha kutokana na ubabe wake, siyo mbabe na hawezi kumfanyia hivyo, kwani angesharudi nyumbani kwao siku nyingi.
“Watu hawajui tu, mie nahisi napendwa zaidi na mke wangu, mimi sio mtu ambaye naweza nikatulia sehemu jambo likiwa limeniumiza. Kwa nini ung’ang’anie sehemu unayoteseka? Hivyo mimi nafurahia maisha nayoishi na mke wangu”, alisema Barnaba.
Huko mitandaoni kulikuwa na tetesi za Barnaba kutokuwa na kauli kwenye ndoa yake, kila anachoambiwa na mke wake kuhusu kufanya kazi za nyumbani na hata kuhusu kitu chochote huitukia kufanya, lakini Barnaba alikanusha tetesi hizo kuwa hazina ukweli wowote bali kuzidiwa kwa mapenzi .
Barnaba ambaye amenyimbo kama, Wrong Number, Nabembelezwa, Milele Daima, Mapenzi Jeneza, amefunga ndoa ya kiislamu na Raya mwaka 2023 baada ya kubadili dini kutoka Mkristo kwenda Muislamu na kuitwa jina la Mohamed