
KLABU ya Simba haikushiriki Mkutano wa kiufundi na Waandishi wa Habari leo kuelekea mchezo wa kesho (Juni 25, 2025) dhidi ya watani wao, Yanga SC Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo hushirikisha Makocha na Manahodha siku moja kabla ya mchezo – na leo Yanga walikuwa peke yao pamoja na Afisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), Karim Boimanda.
Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mualgeria Miloud Hamdi aliongozana na beki wa kati, Dickson Job kwenye mkutano huo ulioanza Saa 5:00 asubuhi.

Mchezo huo wa marudiano wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara unatarajiwa kuanza Saa 11:00 jioni kesho na utaonyeshwa mbashara na Televisheni ya Azam, maarufu kama Azam Tv kupitia chaneli ya Azam Sports 1 HD.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu, lakini ikasogezwa hadi Juni 15 kufuatia malalamiko ya Simba hawatacheza kwa sababu walizuiwa kufanya mazoezi Machi 7, siku moja kabla ya mchezo kwa mujibu wa kanuni.
Bodi ya Ligi ilitangaza rasmi kuuahirisha mchezo huo mchana wa Machi 8, lakini Yanga walikwenda uwanjani na kufanya mazoezi kabla ya kuondoka na baadaye kufungua kesi Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) wakitaka wapewe ushindi.
Hata hivyo, CAS ilikataa kusikiliza kesi ya Yanga kutaka ipewe ushindi na kuagiza irejeshe malalamiko yake kwenye mamlaka za nchini.
Wakati wa sakata hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilikutana na viongozi wa klabu zote, Bodi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ingawa haikuwahi kutoa majibu yoyote juu ya mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Yanga ilikwenda mbali na kutishia kususia hata mechi nyingine mbili za kumalizia msimu dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji pamoja na kujitoa kwenye Ligi ya msimu ujao wapo matakwa yao matatu Kati ya manne hayatatimizwa.
Kwa ujumla uliibuka mgogoro mkubwa baina ya Yanga na TFF – kwani klabu hiyo ilitishia pia kutocheza Fainali ya Kombe la TFF, michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB msimu huu hadi itakapolipwa Fedha zake za zawadi za msimu uliopita.
Fainali ya Kombe la CRDB imepangwa kufanyika Juni 28 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar – Yanga ikikutana na Singida Black Stars.
TFF kwa upande wao walisema ndio wanaidai Yanga na fedha hizo wamekata kufidia madeni hayo.
TFF iliomba kukutana na viongozi wa Yanga kujadili madeni yao ili kinachobaki wapewe, lakini uongozi wa klabu ulikataa na kusema hautaki kikao isipokuwa fedha zao ziingizwe kwenye akaunti yao.
Hata hivyo, mambo yalikaa sawa baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk, Samia Suluhu Hassan kukutana na kuzungumza na viongozi wa Simba na Yanga Ikulu, Chamwino Jijini Dodoma Juni 13 na TPLB ikatangaza kuusogeza mchezo kutoka Juni 15 hadi 25.
Mchezo wa kesho ambao ni kukamilisha msimu- ndio wa kuamua Bingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Yanga SC yenye pointi 79 inahitaji sare tu mbele ya Simba yenye pointi 78 ili kutwaa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.
Kwa mazingaombwe yaliyoanza tena leo, je Simba wataingia uwanjani kesho?