
Mshambuliaji wa Newcastel United, anayesakwa na vilabu vya Liverpool na Arsenal, Alexander Isak ameonywa kuhusu kuongeza mkataba wake kusalia Newcastle wakati huu ambapo amekua lulu na keki Ulaya.
Mwanahabari za michezo, Steve Kay anasema baadhi ya watu ndani ya kambi ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden wanaripotiwa kuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wake wa muda mrefu huko St James' Park na wanamshauri afikirie kwa makini chaguo lake kabla ya kusaini mkataba mpya Newcastle.
Hata hivyo, uwepo wa washambuliaji wengi sokoni katika dirisha la kiangazi, ikiwa ni pamoja na Benjamin Sesko, Viktor Gyokeres, na Victor Osimhen, inaweza kufanya iwe vigumu kwa Isak kupata uhamisho wa ndoto yake ikiwa atasalia Newcastle baada ya dirisha lijalo la uhamisho.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden, 25, amefunga mabao 23 katika mechi 33 msimu huu.
Hugo Ekitike mbadala wa Isak Arsenal?

Arsenal wanataka kumsajili mchezaji wa Eintracht Frankfurt Hugo Ekitike katika majira ya msimu wa joto. The Gunners "wanamtaka" Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 22 kama mbadala wa Alexander Isak kutoka Newcastle.
Newcastle imempa mkataba mpya Mshambuliaji huyo Msweden ambaye amekataa na kama atauzwa itataka dau nono linalofikia pauni milioni 150.
Kwa sababu ya dau hilo kubwa, Ekitike amekuwa mbadala na amekuwa akivivutia vilabu kadhaa vya Ligi kuu Uingereza ambavyo vimeomba kufahamishwa kuhusu kupatikana kwake. Frankfurt wanatarajiwa kuhitaji dau la uhamisho la takriban pauni milioni 60 kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain (Football London).
Gyokeres kuuzwa kwa £50m, Liverpool Arsenal zatajwa

Viktor Gyokeres ataruhusiwa kuondoka Sporting katika majira ya joto, ikiwa ofa ya kati ya £50.2m-£58.5m itatua mezani kwa wareno hao (Skysport).
Klabu yake iko tayari kumuuza, huku vilabu vinavyosaka mshambuliaji kwa sasa zikiwemo Arsenal, Chelsea, Manchester United na Liverpool zitasukumana sokoni kujaribu kupata saini yake katika dirisha la usajili lijalo.
Gyokeres, 26 amekuwa lulu katika ulimwengu wa kandanda hivi sasa. Misimu miwili iliyopita imeonyesha hivyo, akifunga mabao 83 katika mechi 91 katika mashindano yote.
Onana hataki kwenda Uarabuni

Mlinda mlango wa Manchester United, Andre Onana atapuuza ofa nono kutoka timu za Saudi Arabia ili kusalia kama golikipa nambari 1 wa Manchester United.
Kwa mujibu wa Skysport na ESPN kwamba Onana anataka kubaki Old Trafford na atafikiria tu kuondoka ikiwa ataambiwa haitajiki tena. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ana mkataba hadi 2028 baada ya kuwasili kutoka Inter Milan kwa mkataba wa pauni milioni 43.8 mwaka 2023.

Chelsea kumuuza Joao Felix na kumleta Osimhen?
Chelsea wanakaribia kumtoa Joao Felix katika mpango ambao unaweza kufungua milango kwa Victor Osimhen kuhamia Stamford Bridge.
Jorge Mendes, wakala bora anayesimamia mustakabali wa Felix, amethibitisha kwamba Galatasaray wanataka kumsajili mshambuliaji huyo, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo AC Milan kutoka The Blues.
Kwa upande wake, hii inafungua nafasi katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea ambayo inaweza kujazwa na Victor Osimhen, ambaye mkataba wake wa mkopo katika klabu hiyo ya Super Lig unamalizika msimu wa joto na ambaye atauzwa kwa uhamisho wa kudumu na Napoli.