Bill Gates Amlipa Melinda Dola Bilioni 8 Miaka Mitano Baada ya Talaka - IDDYNATION SITE

Breaking News

Bill Gates Amlipa Melinda Dola Bilioni 8 Miaka Mitano Baada ya Talaka

 

Bilionea na mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Microsoft, Bill Gates, amemlipa aliyekuwa mke wake Melinda French Gates kiasi cha dola bilioni 8 za Kimarekani, sawa na takribani shilingi trilioni 23.12 za Kitanzania, miaka mitano baada ya ndoa yao kuvunjika rasmi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Gazeti la The New York Times, fedha hizo takribani dola bilioni 7.88 zilipelekwa kwenye Pivotal Philanthropies Foundation, taasisi ya misaada inayomilikiwa na Melinda, ikiwa ni sehemu ya makubaliano makubwa ya talaka yao.

Mnamo Mei 2024, Melinda alitangaza rasmi kujiuzulu kutoka Bill & Melinda Gates Foundation, taasisi waliyoianzisha na kuiendesha kwa pamoja kwa zaidi ya miongo miwili. Wakati huo, alidokeza kuwa Bill Gates alipaswa kuchangia hadi dola bilioni 12.5 kwa taasisi mpya ya misaada aliyopanga kuanzisha.

Mchango wa sasa wa dola bilioni 8 kwa taasisi ya Pivotal, inayojikita zaidi katika haki, ustawi na maendeleo ya wanawake, unaonekana kuwa ni awamu ya kwanza ya mchango huo mkubwa uliokuwa umependekezwa.

Bill na Melinda Gates walifunga ndoa mwaka 1994 na kuachana rasmi mwaka 2021, baada ya kupata watoto watatu. Talaka yao ilivuta hisia za dunia kutokana na ukubwa wa mali zao na nafasi yao katika masuala ya misaada ya kimataifa.

Baada ya kuvunjika kwa ndoa hiyo, Melinda alimkosoa vikali Bill Gates akihusisha uamuzi wake na madai ya usaliti wa ndoa, pamoja na uhusiano wa karibu wa Bill Gates na Jeffrey Epstein, aliyekuwa mfadhili na mtuhumiwa wa makosa ya kingono dhidi ya watoto.

Kwa upande wake, Bill Gates amewahi kukiri kujutia sana uhusiano wake na Epstein, lakini amekanusha mara zote kuhusika katika vitendo vyovyote visivyo halali.

No comments

Note: only a member of this blog may post a comment.